Mtadanganyika?: Wanachama wa Simba jiepusheni na siasa nyepesi za wagombea. Tumieni muda kutafakari sera za wagombea.
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) baada ya kupokea na kuzingatia maombi ya Simba na kwa kuzingatia Ibara ya 26 ya Kanuni za Uchaguzi za TFF toleo la 2013 limeiruhusu klabu hiyo kuendelea na mchakato wa uchaguzi wao uliopangwa kufanyika Juni 29 mwaka huu.
Hata hivyo, TFF inawahimiza wanachama wa klabu ya Simba kuwa watulivu na wafanye uchaguzi wao kwa amani.
Taarifa hizi kwa asilimia 100 ni njema kwa wanachama, mashabiki, viongozi, wafadhili na wadhamini wa klabu ya Simba sc.
Watu
wote wanaopenda ustawi wa mpira wa nchi hii walitegemea busara za Rais
wa TFF, Jamal Emil Malinzi ambaye alitangaza kusimamisha uchaguzi huo
jumapili iliyopita. Kauli yake ilizua utata miongoni mwa wanasimba na
yakazungumzwa mengi, lakini usikivu wa Malinzi umefanikisha ndoto za
Wanasimba kupata viongozi wao juni 29.
Juhudi
za Rais wa Simba, Alhaj Ismail Aden Rage zimewasha taa ya kijani kwa
Simba baada ya kumuomba Malinzi maandalizi ya uchaguzi yaendelee na
hatimaye kufanyika juni 29 kama ulivyopanga. Ingekuwa mbaya kama
uchaguzi usingefanyika siku hiyo kwasababu klabu inahitaji viongozi ili
usajili uanze na maandalizi ya msimu mpya wa ligi kuu.
Zoezi
linalosubiriwa kwasasa ni kuzinduliwa kwa kampeni ili kila mgombea
anadi sera zake na kuwajulisha wanasimba kwanini anaomba nafasi ya
uongozi.
Nafasi
mbili za juu, Urais na makamu wa Rais zinavuta hisia za wanachama
wengi, lakini kuondoshwa kwa Michael Richard Wambura, kumewaacha Evance
Aveva na Andrew Tupa kupambana.

Simba iliyoifunga Yanga mabao 5-0 ilikuwa yenye ubora, lakini kwa miaka miwili iliyopita, mambo yakekuwa magumu
Safari
ya kuenguliwa kwa Wambura ilikuwa na mizengwe mingi na ilisababisha
mvutano mkubwa ndani ya klabu ya Simba, lakini mwisho wa siku sheria na
kanuni zimetoa jibu.
Ni
imani yangu kuwa utulivu utakuwepo na wale waliokuwa wanamuunga mkono
Wambura watakuwa wavumilivu kwasababu kila unaposhindana lazima ukumbuke
kuna kushinda na kushindwa.
Tatizo
la watu wengi wanawaza kushinda tu, lakini kushindwa wanaona kama ni
dhambi. Penda kushindwa, halafu jipange upya. Ukiwa mtu wa kuwaza
kushinda tu, ukishindwa `unapaniki` na hatimaye kushindwa kabisa
kabisa!.
Wanachama
wa Simba mnatakiwa kuvunja kundi la Wambura na kushirikiana kwa pamoja
ili juni 29 mpate mtu atakayewaunganisha na kuifanya Simba kuwa imara.
Naamini uchungu mlioupata kwa miaka miwili sasa unatosha na kuna haja ya
kuijenga Simba ya ushindani.
Kwa kuanzia, lazima mpate viongozi sahihi, wenye mtazamo sahihi na watakowafanya mpige hatua kwenda mbele.
Kampeni
zinaanza juni 24 mwaka huu kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na kamati
ya uchaguzi chini ya wakili, Dkt. Damas Daniel Ndumbaro.
Niwakumbushe
kitu kimoja tu,kampeni ni nafasi ya mgombea kunadi sera, mipango na
kueleza kwanini anagombea. Pia anaweza kueleza jinsi atakavyotekeleza
sera zake na kufanikiwa.
Katika
chaguzi za kidemokrasia, Kampeni ndio muda unaowafanya watu wapate
viongozi bora na bomu. Hapa ndipo siasa ilipolalia. Ushawishi huwa ni
mkubwa na kudanganywa pia kupo.
Wanachama wa Simba sc juni 29 mwaka huu mna mamlaka makubwa kikatiba kuamua nani aingia na nani atoke.
Mara
nyingi, wagombea wengi wanapenda kuongea mambo yanayovutia na
kushawishi. Usipokuwa makini unaweza kumchagua mtu mwenye maneno mazuri,
lakini ikifika wakati wa utekelezaji, mambo yanageuka.
Najua
kwa muda wote huu, wagombea wote wamekuwa wakiandika na kuandikiwa cha
kuzungumza mbele ya wanachama wa Simba. Najua yatazungumzwa mengi kutoka
kwa wagombea, lakini umakini wa wanachama ndio utachambua mtu sahihi wa
kumpa kura.
Wapo
watakaosema lazima wajenge uwanja wa kisasa, wauze jezi za klabu kwa
faida ya timu, wataifanya klabu kuwa bora uwanjani kwa kusajili
wachezaji wazuri, kuifanya Simba ijitegemee na mengine mengi.
Sina shaka na mtu atakayesema haya kati ya mengi yatakayosikika. Najua kweli Simba inahitaji mambo kama hayo na mengine mengi.
Lakini
mwisho wa siku, kuna kitu kinaitwa `sera au ahadi zisizotekelezeka`.
Hapa lazima wanachama wa Simba kuwa makini ili msije kujenga imani kubwa
na mgombea fulani kwasababu ya sera zake, kumbe hazitekelezeki.
Lazima
upime uwezo wa klabu yenu kifedha, halafu pima uwezo wa mgombea
anayezungumza, halafu dadavua kama kweli anaweza kufanikiwa
anayozungumza.
Sisemi
uwezo wa kifedha hapa, nazungumzia utashi, uimara na ujanja ujanja wa
kutafuta njia za kupata fedha kwa faida ya Simba. Mgombea mwenye uwezo
wa kuhangaika kwa ajili ya klabu kwa kuzungumza na makampuni, wadhamini
na wafadhili ili aitunishe akaunti ya timu kwa matumizi tofauti tofauti.
Moja
ya siri ya kufanikiwa kwa kiongozi ni kuchagua mambo machache kwa muda
ulionao na kuyatekeleza ipasavyo. Lakini kwa siasa za Tanzania, mgombea
anaahidi mambo 10 anatekeleza matatu au hatekelezi yote. Ikifikia wakati
wa uchaguzi anajipanga na uongo mwingine.
Kiongozi
bora ni Yule anayekuwa na malengo machache ndani ya muda mfupi. Kwa
kipindi cha miaka minne ya uongozi, anajikita kwenye ahadi zake chache
na akiweza, atajijengea heshima.
Wanachama
wa Simba, pimeni sera za wagombea wenu na kuzichambua kama
zinatekelezeka. Msije mkajidanganya na kuwaamini kwa maneno ya mdomoni,
lakini kiuhalisia hayawezekani.
Alhaj Ismail Aden Rage anaondoka madarakani na amefanya kazi nzuri kuhakikisha uchaguzi unafanyika tarehe iliyopangwa.
Wapo
watu kazi yao ni kuandaa sera za wagombea. Wana uwezo mkubwa wa kuandaa
mipango yenye mvuto, lakini utekelezaji wake unakuwa mgumu kwasababu
wanaandika tu bila kuangalia mazingira ya pale wanapoenda kuongoza.
Maneno si kigezo cha kumuamini mtu, lazima ujua anawezaje kufanikiwa kwa mazingira mliyonayo kwenye klabu.
Kwa
wagombea, ogopeni kudanganya watu wazima. Kama kweli mna nia ya dhati
kuindeleza klabu ya Simba, njooni na sera zinazotekelezeka na ambazo
zipo chini ya uwezo wenu. Sio mnakuja na mambo mazito ambayo Simba
haiwezi kuyabeba.
Kama
mtadanganya na kushindwa kufikia malengo yenu, mjiandae kuingia katika
orodha ya wanasiasa waliovamia mpira bila kuwa na nia ya kweli. Ni imani
yangu kuwa mmeomba nafasi kwasababu mnataka kufanya kazi nzuri.
Simba inahitaji mabadiliko baada ya kupitia kipindi kigumu cha miaka miwili. Kila atakayepewa nafasi, basi awajibike vizuri.
Wanachama
wa Simba, juni 29 mna mamlaka makubwa kikatiba. Ninyi ndio mtashika
rungu na kuamua nani anaingia nani anatoka. Msichague kwa kushawishika
na wenzenu.
Kura
ni siri ya mtu na lazima iwe siri. Kama mtu anatoka ndani ya chumba cha
kupigia kura anatakiwa aendelee na mambo yake, sio anamwambia mwenzake,
mimi nimemchagua fulani, nawewe kumchague. Kila mtu aingie kivyake na
kufanya yake
Kila la heri wana Simba kuelekea uchaguzi wenu wa Juni 29. Amani na iwe nanyi kwa wakati huu muhimu.
chanzo: mpenja blog.
0 comments:
Post a Comment