Dodoma. Mke wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, mama Tunu Pinda amesema kuwa alishtuka kusikia habari kwamba mumewe ametangaza nia ya kuwania urais mwaka 2015.
Magazeti mbalimbali, yaliandika habari zilizodai kuwa Pinda ametangaza nia kutaka kuwania urais mwaka 2015. Hata hivyo, katika mahojiano na gazeti hili juma lililopita, Waziri Mkuu Pinda alisema kuwa kutajwa kutaka kuwania nafasi hiyo ni jambo jema na kutangaza nia pia ni jambo jema.
Lakini katika mahojiano na gazeti hili yaliyofanyika nyumbani kwake mjini Dodoma, Tunu Pinda alisema:
“…Niliposikia kwanza nilishtuka kwa sababu bahati mbaya hatukuwa pamoja nikajiuliza imekuwaje. Ukweli nilishtuka na alipokuja nikamuuliza, naye akasema; “mimi sijatangaza, wala sijaita vyombo vya habari au labda kuzungumza kwamba nautaka urais, lakini muda utakapofika nitasema.”
Tunu ambaye mwezi uliopita aliteuliwa kuwa Balozi wa Amani Duniani na mkutano wa dunia (World Summit 2014), ulioandaliwa na Taasisi ya Universal Peace Federation(UPF), nchini Korea Kusini aliongeza:
“Kwa hiyo kama walivyosema na iwe hivyo kama Bwana Mungu aishivyo, nasema amina. Kwa sababu muda bado haujafika, utakapofika tutajua.”
Uwaziri Mkuu wa Pinda
Akizungumzia nafasi ya uwaziri mkuu kwa Pinda aliyodumu nayo tangu mwaka 2008, mke huyo wa Waziri Mkuu alisema, mumewe ameweza kudumu na kuwa salama hadi sasa kwa nguvu na uwezo wa Mungu.
“Yaani unamwona huyu bwana (Pinda), mpaka leo kwenye nafasi hii ni kwa ajili ya nguvu na neema za Mungu. Kwa akili za kibinadamu huwezi. Bila kumtarajia Mungu afanye, hutaweza. Kwa hiyo tuna ratiba ya kusali kifamilia kila siku na kushiriki kusali kanisani na kujitolea kama watu wengine,” alisema Tunu.
Majukumu yake kama mama
Akizungumzia majukumu yake kama mama awapo nyumbani, mke huyo wa Waziri Mkuu alieleza kuwa maisha yake ni ya kawaida kama mama mwingine wa Kitanzania aliye na majukumu ya kifamilia.
“Maisha yangu ni ya kawaida sana si kwamba kwa nafasi niliyonayo niishi maisha ya ajabu, hapana. Kinachoongezeka kwangu ni kule kuwa mke wa kiongozi, labda na taratibu zinazoendana na nafasi hiyo,”alisema Tunu.
Tunu anayefahamika pia kwa jina la Petronila alisema kuwa akiwa nyumbani pamoja na mambo mengine hujishughulisha na kilimo pia ufugaji nyuki, akieleza kuwa hupanga ratiba kwa ajili ya kazi zake binafsi, ratiba za Waziri Mkuu pia kuangalia familia.
“Kwa familia, nikiwapo natumia muda huo kuzungumza na kila mtoto kujua kama ana matatizo au la. Kila jioni husali kwa pamoja na baada ya hapo hupata nafasi ya kuzungumza nao na kujua kama tupo salama au wana matatizo na namna ya kuyatatua matatizo yanayojitokeza,”alisema na kuongeza:
“Lakini kama mke wa kiongozi pia nina ratiba zangu, mara nyingi kama naletewa ratiba ya mambo ya kushiriki, lazima niangalie na ratiba ya mheshimiwa (Pinda) ili zisije zikagongana.
Inaweza kutokea mzee anahitajika mahali awe na mimi, lakini hutokea kila mmoja awe na ratiba yake. Pengine yeye yuko Dodoma, mimi Dar es Salaam kwa ratiba ya kikazi na zikapita siku kadhaa.”
Inaweza kutokea mzee anahitajika mahali awe na mimi, lakini hutokea kila mmoja awe na ratiba yake. Pengine yeye yuko Dodoma, mimi Dar es Salaam kwa ratiba ya kikazi na zikapita siku kadhaa.”
Kuhusu changamoto za kifamilia mama Pinda anasema:
“Changamoto ninayoipata wakati mwingine, naweza kuwa na suala la kifamilia na ninataka kumshirikisha mheshimiwa (Pinda), sasa hapo lazima uangalie yupo kwenye hali gani. Hivyo lazima kuangalia muda gani wa kumshirikisha maana siyo kila siku ni Krismasi.”
Aliongeza: “Hivyo, hapo lazima nipambane mwenyewe na kutumia hekima ya kimama kutatua tatizo, baada ya hapo unamshirikisha na kama kuna la nyongeza basi naye anasema. Kwa hiyo tuna ratiba ya kifamilia na sisi kushiriki mambo ya kijamii hata ya kujitolea na kanisani kama watu wengine.”
Sifa za urais
Akizungumzia sifa za mtu anayefaa kuwa rais alitaja ya kwanza kuwa ni uadilifu, uzalendo na hofu ya Mungu, pia anayeweza kulifikisha taifa la Tanzania mahali pazuri zaidi.
“Kitu cha kwanza lazima awe mzalendo kwa maana ya Mtanzania, awe mwadilifu. Unajua kiongozi ni kioo ili anaowaongoza waige mazuri kutoka kwake, lakini vile vile awe mchapakazi na kwa sababu mimi ni mwanaCCM, awe mwanaCCM ambaye tunaamini anaweza kutufikisha pazuri, awe mpenda watu.
Sifa ni nyingi tu, awe na hofu ya Mungu, naamini mwenye hofu hiyo atatuongoza vizuri. Mungu amekuwa akiteua viongozi na wanaomtegemea yeye wanafanya vizuri, hiyo iwe sifa ya kwanza,” alisema mama Tunu.
Uchaguzi Mkuu 2015
Akizungumzia uchaguzi mkuu ujao mwaka 2015 na nafasi ya wanawake katika uongozi, mama Pinda aliwataka wasitegemee nafasi za kuteuliwa akitoa wito kwa wanawake kujitokeza kuwania nafasi za uongozi kuanzia ngazi ya mitaa, vitongoji hadi taifa akiwataka kuunga mkono wenzao watakaowania nafasi hizo.
Katiba Mpya
Kuhusu mchakato wa Katiba na muundo wa Serikali, alisema:
“Mimi mtazamo wangu haupo hata kwenye mapendekezo ya Rasimu. Mtazamo wangu kama Tunu nilitamani sana iwe Serikali moja. Kwa kuwa moja haipo, hata kwenye rasimu, tuendelee hivi tulivyo sasa hivi.
Tuendelee kuishi kindugu, yale matatizo yaliyo kwenye Muungano yaendelee kurekebishwa. Tuhakikishe tunaendelea kudumisha undugu wetu kwa miaka mingine hamsini ijayo.”
Balozi wa Amani Duniani
Agosti 12,2014 Mama Pinda alitunukiwa tuzo na kuteuliwa kuwa Balozi wa Amani Duniani katika mkutano uliojadili amani, usalama na maendeleo ya dunia ulioandaliwa na UPF, inayotoa ushauri kwenye Baraza la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Uchumi na Jamii ambapo pia alikuwa mmoja watoa mada.
Akinukuu alichosema katika mkutano huo uliokuwa wa siku tano na kujumuisha wajumbe nchi 68 duniani kote na aliwasilisha mada iliyohusu amani, maendeleo kwa binadamu barani Afrika alisema:
“Naiomba jamii ya kimataifa duniani tusimamie amani na usalama, kinyume na hapo ni kuleta machafuko. Wanawake hatupendi vita, wala machafuko.
“Nawasihi tuendeleze maono ua Muumba wetu, Tuweke utu mbele kwa kuwajali wengine, tuache kutanguliza masilahi binafsi,” alisema mama Pinda na kuongeza:
“Nilitaka washiriki wote tusimame kwenye nafasi zetu kama baba, mama, kaka na dada kuhakikisha dunia inakuwa mahali pazuri pa kuishi.”
Alisema kuwa katika mkutano huo mwasilishaji kutoka Afrika alikuwa pekee yake ambapo alizungumzia usalama na amani Afrika Mashariki, ukanda wa Sadc, Bara la Afrika na dunia.
“Kama hakuna amani, hakuna maendeleo na hamwezi kupanga maendeleo kwa sababu muda wote hakuna uhakika na usalama wenu. Kwa hiyo usalama na amani ni vitu muhimu kwa mustakabali wa maendeleo ya nchi na binadamu. Binadamu anastahili vitu hivyo ndipo ataweza kufikiria maendeleo.
Binadamu ana haki ya kuishi kwa amani na wanaothirika amani inapokosekana ni kinamama, watoto na wazee wao hukosa uwezo wa kukimbia. Natamani dunia izungukwe na amani ili tuweze kuleta maendeleo kwani Mungu hakutuumba ili tuteseke,”alisema.
Binadamu ana haki ya kuishi kwa amani na wanaothirika amani inapokosekana ni kinamama, watoto na wazee wao hukosa uwezo wa kukimbia. Natamani dunia izungukwe na amani ili tuweze kuleta maendeleo kwani Mungu hakutuumba ili tuteseke,”alisema.
0 comments:
Post a Comment