Wednesday, 1 October 2014

MAJANGA:BMW LA WEMA SEPETU UTATA MTUPU


Achana na lile gari aina ya Nissan Murano alilozawadiwa na mwandani wake, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, gari lingine aina ya BMW 545i aliloletewa Wema Isaac Sepetu ‘Beautiful Onyinye’ kwenye pati ya ‘bethidei’ yake ni utata mtupu na maswali kibao.
Wema Isaac Sepetu ‘Beautiful Onyinye’ akiwa ndani ya Gari aina ya BMW 545i alilozawadiwa na meneja wake.
NYUMBANI KWA MADAM
Pati hiyo ambayo iliandika historia katika ulimwengu maridhawa wa mastaa iliangushwa nyumbani kwa mwanadada huyo, Mtaa wa Bwawani, Kijitonyama jijini Dar, wikiendi iliyopita ambapo alitimiza umri wa miaka 26.
Katika shughuli hiyo, waalikwa ambao sehemu kubwa walikuwa watu wenye majina, walikula na kunywa kuanzia mchana hadi usiku mnene.
NISSAN MURANO
Akiwa Marekani, Diamond alimuagiza mama yake, Sanura Kassim ‘Sandra’ apeleke gari aina ya Nissan Morano lenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 36 za madafu ikiwa ni zawadi ya jamaa huyo kwa mkewe huyo mtarajiwa.
Gari aina ya BMW 545i alilozawadiwa Wema Isaac Sepetu ‘Beautiful Onyinye’ na meneja wake.
Alipoliona gari hilo, Wema alipigwa na butwaa huku akimshukuru Diamond ambaye kwa sasa amempachika jina la Chibu baada ya lile la Dangote ‘kueksipaya’.
MANENO KUNTU
Huku akiambatanisha na picha ya gari hilo, kupitia ukurasa wake wa Instagram alimwandikia Wema: “Nilitazama nikupe vingi huenda ingesaidia kukueleza ni kiasi gani napenda nikuone ukiwa umefurahi kwenye siku yako hii ya kuzaliwa...lakini tu sina uwezo huo Mumy...tafadhali pokea hicho kidogo hiki nilichojaliwa leo.”
BMW UTATA MTUPU!
Gari aina ya BMW alilokabidhiwa na meneja wake, Martin Kadinda ndilo habari ya mjini huku nyuma yake kukiwa na maswali kibao.
Martin Kadinda akionyesha funguo ya Gari aina ya BMW aliyomzawadia Wema.
MAMA WEMA AHOJI
Wa kwanza kuhoji alikuwa ni mama mzazi wa Wema, Mariam Sepetu ambaye alikataa kwamba Kadinda hawezi kutoa zawadi ya gari kama hilo hivyo minong’ono ikawa ni mingi.
Baada ya kuona hivyo, Kadinda alitoa kadi ya gari hilo lenye namba spesho za usajili ambapo jina la mmiliki lilisomeka Wema Sepetu.
MKONGO ATAJWA
Hata hivyo, pamoja na utetezi wake, maneno yaliendelea kusambaa kama moto wa kifuu kwamba nyuma ya gari kuna stori kubwa inakuja.
Muonekano wa keki ya ‘bethidei’ ya Wema.

Minong’ono mingine ilikwenda mbele zaidi huku jamaa mmoja mfanyabiashara kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (Mkongomani) akitajwa kulinunua na kumpa Kadinda akakabidhi.
Baada ya kuona gari hilo lenye thamani ya zaidi ya Sh. Milioni 56 za madafu zinaleta utata, kama kawaida yake, Kadinda alikimbilia kwenye ukurasa wake wa Instagram akaandika:
“....Gari hili linatokana na kazi ndogo tuzifanyazo na sapoti kubwa ya watu wanaotutakia mema. Peke yangu nisingeweza bila sapoti yao....”
Wema Isaac Sepetu ‘Beautiful Onyinye’ akimlisha keki mama yake.
MSISITIZO
Akizungumza na gazeti hili juu ya sakata hilo, Kadinda alisema kwa msisitizo: “Ni mimi ndiye nimemnunulia Wema hilo gari.”
MASWALI
Huku Kadinda akisisitiza hivyo, waalikwa walibaki na maswali vichwani likiwemo lile linaloulizwa zaidi kwamba iweje yeye (Kadinda) aendeleshe gari la thamani ndogo aina ya Toyota Corola halafu ampe Wema BMW?
“Hapa pana kitu na kitakapobumburuka itakuwa soo, ni bora Kadinda angefunguka ukweli kuliko kuja kunyooshewa vidole baadaye, ngoja tusubiri,” alisikika mmoja wa mastaa walioalikwa (jina kapuni).
Akimlisha keki mamamkwe wake.

MENGINE YATOKANAYO
Pati hiyo ya Wema iligawanyika mara mbili ambapo ya kwanza ilianza saa 6:00 mchana hadi saa 12:00 huku nyingine iliyohusisha watu maarufu ikianza baadaye hadi ‘kokoriko’.
KEKI 69 MEZANI
Katika hali isiyo ya kawaida, sherehe hiyo ilikuwa na keki zipatazo 69 ambazo zililetwa na baadhi ya mastaa ambao walihudhuria sherehe hiyo huku kukiwa na vinywaji vya kufa mtu (wiski tu), loko bia tupa kule.
Akimlisha keki Jokate.
NDAFU
Kwa upande wa nyama kulikuwa ndafu mzima ambaye watu walimtafuta hadi wakasaza.

MAMA DIAMOND AMTANGAZA RASMI MKWEWE  
Katika sherehe hiyo, mama Diamond alipopewa kipaza sauti ‘maiki’ ili anene chochote alisema kuwa Wema ni mkwe wake wa halali na kwamba anampenda hivyo asiwe na wasiwasi kwani hakuna mkwe mwingine atayatokea zaidi yake.
Wema Sepetu ‘Beautiful Onyinye’ akifungua shampeni kwaajili ya shughuli hiyo.
“Jamani huyu ndiye mkwe wangu, Mrs Chibu (Diamond) ndiye mkwe wangu hasaaa...,” alisema mama Chibu huku watu wakishangilia.
MILIONI 10
Kwa mujibu wa Kadinda, shughuli hiyo iligharimu zaidi ya Sh. milioni 10 hadi kukamilika na kuonekana ya tofauti na pati nyingine za mastaa Bongo.
Wema akiongea jambo kabla ya kukata Ndafu.
AMWAGIWA NOTI

Ulipofika muda wa kutunzwa zawadi, watu walijitokeza kumtunza Wema fedha ambazo hazikuweza kupatikana kiasi chake mara moja huku staa wa sinema za Kibongo, Elizabeth Michael ‘Lulu’ akiweka rekodi kwa kumwaga ‘minoti’ mingi katika hafla hiyo.
Imeandaliwa na Imelda Mtema, Shani Ramadhan na Mayasa Mariwata.

0 comments:

Post a Comment