IDADI ya wagombea nafasi ya Urais kupitia CCM sasa imefikia 28 baada ya jana makada wengine sita kuchukua fomu.
Waliochukua fomu jana ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, Naibu Waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia, January Makamba, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, mkazi wa Musoma mkoani Mara, Boniface Ndengo na mkulima kutoka Kijiji cha Mjimtala wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, Eldefonce Bilohe na Dk Hassy Kitine.
Wengine waliochukua fomu ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, Dk Mwele Malecela, Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kingwangala, Balozi, Amina Salum Ally, Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, Waziri wa Kilimo na Chakula, Steven Wassira, Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal na Waziri wa Ujenzi, John Magufuli.
Wengine ni Balozi Ally Karume, Mbunge wa Kisesa Luhaga Mpina, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi Maalumu, Profesa Mark Mwandosya, Mtumishi wa CCM Idara ya Siasa na Uhusiano wa Tanzania Amos Siyantemi, Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, Wakili mwandamizi Mahakama Kuu Tanzania Godwin Mwapango, Peter Nyalile, Leonce Mulenda, Wengine Sospeter Muhongo, Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Titus Kamani, Makongoro Nyerere na mwanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, Amos Robert.
Wagombea wanaotarajia kuchukua fomu leo ni Agustino Mahiga na Monica Mbega. Dk Kitine asema anaiogopa Ikulu Akitangaza jana nia yake, Dk Kitine aliwataka Watanzania kutokataa fedha wanazopewa na baadhi ya wagombea na watangaza nia ya urais, kwani ni mali ya umma walizoibiwa.
Kauli ya Kitine ameitoa jana mjini hapa wakati wa kutangaza nia yake ya kujitosa katika kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM). “Kuna baadhi ya watu wamekuwa wakitumia fedha za umma walizoziiba kuwanunua watu wa kuwaunga mkono na baadhi ya vyombo vya habari ili waonekane wanakubalika kwa jamii.
Hivyo wakija kwenu na kuwapa fedha chukueni hizo ni fedha za umma. “Mtu anatangaza nia anajaza uwanja wa mpira, kwa kutumia fedha hivi kweli mtu huyo akipata urais na kwenda Ikulu si lazima atake kurudisha fedha zake, wakati Ikulu sio sehemu ya kufanyia biashara,”alisema.
Kitine pamoja na kuiogopa Ikulu, lakini yeye amejitafakari kwa kina kabla ya kufikia uamuzi wa kutangaza nia ya kugombea nafasi hiyo. “Binafsi anaiogopa sana Ikulu na hii ndio mara yangu ya kwanza najitokeza kuzungumzia hili, lakini mpaka nimefikia uamuzi wa kutangaza nia ya kugombea, mjue nimejitafakari kwa kina,” alisema.
Alisema nafasi ya wanayoitafuta ya kuwania urais ni kubwa mno, na kuwa ni tofauti na wanavyofikiria wagombea wengine aliowaita wenzie wanaotaka kuingia eneo takatifu. “Mtu anayetaka kwenda Ikulu kwa lazima hafai, mimi napafahamu sana ndio mana naona taabu... ninaogopa sana,” alisema.
Alisema endapo atapata ridhaa ya chama atajitahidi kumkaribia utendaji wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. “Siwezi kufanana na Mwalimu Nyerere ila nitajitahidi kumkaribia, kwani alipitishwa na CCM ambayo inaweza kumteua kiongozi mwingine mzuri kama huyo.
Alisema pia endapo apata ridhaa hiyo atatekeleza ilani ya CCM kwa uaminifu, uadilifu pamoja na uwazi. Chikawe kupambana na maadui watatu Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu, Chikawe alisema endapo anapewa ridhaa ya kuongoza, atahakikisha anapambana na maadui watatu wa asili ambao ni ujinga, maradhi na umasikini na pia adui mbaya rushwa kwa kuendeleza misingi iliyowekwa na marais wa awamu zote nne.
“Tangu Uhuru, CCM imekuwa ikipambana na maadui watatu wa taifa ambao ni ujinga, maradhi na umasikini na hivi sasa kuna adui mbaya rushwa ambaye amekuwa akidhoofisha juhudi za kupambana na maadui wa kwanza watatu. “Marais wa awamu zote nne wameweka misingi ya kupambana na maadui hawa, hivyo misingi hiyo itaimarishwa, itaboreshwa na kuwekewa mikakati mipya inayoendana na changamoto za sasa ili kuendelea kupambana vikali dhidi ya maaduhi hawa wakubwa,” alisema.
Akijibu swali la kama ana jipya gani zaidi ya wagombea wengine, Chikawe ambaye alikuwa ameambatana na mkewe Profesa Mandina Lihamba alisema kuwa ahatakikisha anatekeleza wajibu wake wa urais kwa kuzingatia sera na ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 kupitia uongozi wa wazi na shirikishi.
“Mimi ni mwanachama muadilifu wa CCM na ninaomba fursa ya kuteuliwa na chama niwe katika nafasi ya urais ili niongoze utekelezaji wa sera ya chama changu serikalini.
Aliongeza: “Jambo muhimu kwangu si tu nitafanya nini nikipata ridhaa ya chama lakini zaidi ni jinsi gani kwa kupitia uongozi wa wazi na shirikishi nitaongoza utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2015 kwa ubinifu, uthabiti, uzalendo na umakini mkubwa kwa faida ya maendeleo ya taifa na watanzania tunaowatumikia.
Ninaisubiri fursa hiyo adhimu nipo tayari kukabiliana na changamoto zote.” Alipotakiwa kueleza ni namna gani atashughulikia tishio la ugaidi akipata nafasi hiyo, Chikawe alisema tangu ameingia kwenye wizara aliyopo sasa, matishio na matukio yenye viashiria vya kigaidi yamedhibitiwa bila kuwaeleza wananchi mbinu zisizotumika na kuwahakikishia watanzania kuwa wataendelea kuwa salama endapo atashika wadhafa huo.
“Nimeingia wizarani Januari mwaka jana, na huko nyuma kulikuwa na matukio ya milipuko ya mabomu huko Arusha na maeneo mengi, lakini sasa hali hii hamuisikii kabisa, hauwezi kuweka hadharani mbinu zinazotumia kupambana na hali hiyo, ila niwakikishie watanzania kuwa watakuwa salama nikiwa rais,” alisema.
Ngeleja: Mimi ni mtu safi Kwa upande wake Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja jana alichukua fomu za kugombea Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mpinduzi (CCM) na kusisitiza kuwa yeye ni mtu safi na hahusiki na ubadhirifu wowote licha ya kutajwa kwenye kashfa mbalimbali.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana, alisema yeye ni mtu safi kwani hana tuhuma zozote ambazo zilimtia hatiani licha ya kuzushiwa masuala mengi.
Alipoulizwa swali na mmoja wa waandishi wa habari kwa nini ameamua kugombea nafasi kubwa katika nchi ya Urais kutokana na kukumbwa na kashfa mbalimbali ambazo zilimsababishia kuondolewa kwenye nafasi wa Uwaziri wa Nishati na Madini, Ngeleja alisema hizo zilikuwa ni tuhuma tu ambazo mwisho wa siku alionekana kuwa hana hatia.
“Pamoja na kuhusishwa maeneo mengi sijawahi kuthibitishwa nina upungufu wa uadilifu kwa mujibu wa misingi ya haki,” alisema. Alisema katika dunia iliyojaa ushahidi tele kwa baadhi ya mambo ambayo yanazuliwa kuna uwezekano kwa watu kufanya hivyo kwa maslahi yao na hata kuamua wanalodhani,” alisema.
Ngeleja alisema kumekuwa na uzushi mwingi kutokana na watu kutokuwa na taarifa sahihi. “Nasema kwa kujiamini sina kasoro na sijawahi kudhibitika,” alisema.
Alisema ukiwa binadamu huwezi kuacha kuhusushwa na jambo moja au lingine. Akitoa mfano alisema mwaka 2004 Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini alizushiwa kashfa ya uuzaji wa silaha na msimamizi wake alifungwa, alifukuzwa Chama cha ANC lakini haki ilitamalaki.
“Rais Zuma alirudi kwa kusaidiana na wenzake na leo ni Rais kwenye haki uongo na fitina vinajitenga,” alisema. Pia alisema kuhusu suala la Escrow alisema akiwa mbunge kupata misaada si jambo la ajabu.
Makamba anaamini CCM itatenda haki Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Tekinolojia, January Makamba amechukua rasmi fomu za kuwania nafasi ya urais huku akisisitiza kuwa na imani na viongozi wa chama hicho na utaratibu mzima wa uteuzi wa mgombea urais unaotumiwa na chama hicho.
Makamba alichukua fomu hizo huku akiwa amesindikizwa na mkewe na wazazi wake ambao ni mama yake na baba yake aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba.
Akizungumza na waandishi mara baada ya kuchukua fomu hizo, alisema ana imani kubwa na utaratibu wa chama hicho wa kupata mgombea urais kutokana na ukweli kuwa pamoja na utaratibu huo kuwepo tangu enzi za Mwalimu Nyerere lakini pia ni wa uwazi, usio na mashaka na unaozidi kuimarika.
“Lakini pia nina imani na viongozi wakuu wa chama changu kuwa watazingatia haki katika kutekeleza utaratibu huu wa kuteua mgombea atakayewakilisha chama chetu,” alisisitiza.
Alisema hakuomba nafasi hiyo kwa kujaribu bali ni kwa nia ya dhati aliyonayo ya kuiletea Tanzania mabadiliko. “Ninaamini mimi naweza kuiletea ushindi CCM katika uchaguzi mkuu ujao, uwezo, ukomavu, nia na dhamira nnayo kulifanikisha hili.”
Imeandikwa na Anastazia Anyimike na Sifa Lubasi
0 comments:
Post a Comment