Saturday 25 October 2014

DARASA LA MAPENZI:JE MPENZI WAKO AMEKUSALITI?? SOMA HAPA KUPATA SOMO




MAPENZI yamegeuka shubiri, usaliti na maumivu ya moyo yamegeuka na kuwa
sehemu ya kawaida katika uhusiano wa kimapenzi. Zaidi ya asilimia 50 ya wanandoa, wanalia kuwa wanasalitiwa au waliwahi kusalitiwa na wenzi wao, si wanawake, si wanaume.
Zipo sababu nyingi zinazosababisha usaliti lakini lengo langu leo siyo kuzungumzia hilo bali ni kujaribu kuiponya mioyo ya wanandoa au watu wanaoishi kwenye uhusiano wa kimapenzi, waliojeruhiwa na usaliti.
Yawezekana ulitokea kumpenda sana mwenzi wako, ukaamini wewe ndiyo kila kitu kwake, ukamtimizia kila kilichokuwa ndani ya uwezo wako lakini mwisho, ukaambulia maumivu baada ya kugundua kuwa yupo mwingine anayekuibia mali zako.
Tujenge hoja! Vitabu vya dini mbalimbali vinaeleza kuwa kosa pekee linaloweza kuivunja ndoa, hata ile iliyofungwa kwa baraka za Mungu, iwe ni madhabahuni au msikitini, ni USALITI.
Sitaki kupingana na maandiko hayo lakini nataka tujadiliane, ni lazima kila unapogundua kuwa mwenzi wako amekusaliti dawa yake ni kupeana talaka au kuachana kwa ugomvi? Dunia imebadilika, wanaume wengi wanasaliti ndoa zao kwa sababu moja au nyingine, hali kadhalika wanawake.
Mathalani umefunga ndoa na kuishi na mwenzi wako kwa kipindi kirefu mkipendana, kujaliana na kuoneshana kila aina ya mahaba lakini akateleza na kukusaliti ilihali bado anakupenda, utakapoamua kuachana naye na kwenda kwa mwingine, ukigundua naye anakusaliti utafanya nini? Utaachana na wangapi? Utaolewa na kuachika mara ngapi?
Bila shaka umeanza kunielewa kwamba siyo mara zote talaka au kuachana ndiyo suluhisho la usaliti ndani ya ndoa. La hasha! Siwafundishi watu wasaliti ndoa zao au uhusiano wao kwa makusudi wakitegemea kusamehewa, hapana.
Ninachotaka kukijengea hoja ni kwamba, hata baada ya mwenzi wako kukusaliti, bado mna nafasi ya kuendelea na maisha yenu ikiwa tu mtaamua kulishughulikia tatizo hilo kwa kina bila kujali watu wa nje wanasemaje.

Usikilize moyo wako, ni kweli amekusaliti! Amekuumiza, unahisi dunia yote imekuelemea, unatamani kufa au kuua, lakini je, moyo wako unakuambia nini? Upo tayari kumruhusu mwizi wako ndiyo awe mmiliki halali wa mwenzi wako ambaye umetumia muda mrefu kumjenga awe vile unavyotaka?
Jibu sahihi halitapatikana kwa kukurupuka, hakuna uamuzi wa busara unaotoka ukiwa na hasira, jazba au ukiwa na shinikizo kubwa kutoka kwa marafiki, ndugu, majirani na watu wanaokuzunguka.
Pata muda wa kurelax kisha usikilize moyo wako, majibu yatakayotoka ukiwa umetulia, ndiyo yatakayoamua kama uendelee au usiendelee na uhusiano uliosababisha ukaumia.
Yawezekana wewe ndiyo ulikuwa sababu ya mwenzako kuchepuka, au ni tamaa za kimwili ndizo zilizomsukuma kuyafanya hayo, lakini jambo la msingi ni kujiuliza; bado anakupenda? Anaonesha kujutia makosa yake? Anakiri na kukuomba msamaha? Kabla hajakusaliti, mmefanya mambo mangapi mazuri? Tuliza akili kisha amua.

0 comments:

Post a Comment