Friday, 3 October 2014

BUNGE LA KATIBA: KURA MBILI ZAPITISHA RASIMU YA KATIBA


Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Deo Sanga akisakata muziki katikati ya
Ukumbi wa Bunge hilo baada ya kutangazwa kwa matokeo ya kura zilizopigwa kupitisha Rasimu ya Mwisho ya Katiba inayopendekezwa mjini Dodoma jana.
Licha ya upinzani kutoka makundi kadhaa ya wananchi, Bunge la Katiba jana lilihitimisha kazi yake kwa kupitisha Katiba inayopendekezwa baada ya kupata theluthi mbili za wajumbe wa kila upande wa Muungano.

Matokeo hayo yaliyohitimisha mchakato huo, yalifanikishwa kwa tofauti ya kura mbili za wajumbe katika baadhi ya ibara na nyingine kwa kura moja tu, ikimaanisha kuwa iwapo kura hizo mbili zingekosekana hadithi ingekuwa tofauti.
 Kutangazwa kwa matokeo hayo kuliwafanya wajumbe walioshiriki mchakato hadi hatua ya mwisho baada ya wenzao wa kundi la Ukawa kususia, kulipuka kwa furaha, nyimbo, tambo, vijembe na vigelegele huku wakijimwaga ukumbini kusakata dansi.
Akitangaza matokeo hayo, Naibu Katibu wa Bunge hilo, Dk Thomas Kashililah alisema hali ya upigaji kura ilikuwa ni nzuri na kila kura za kila upande zilitosheleza na kutoa uhalali wa Katiba inayopendekezwa kupelekwa kwa wananchi.
Katibu huyo alianza kutoa matokeo ya upande wa Zanzibar ambako wajumbe wengi walikuwa na wasiwasi kuwa huenda usipate akidi ya kura 146 iliyotakiwa.
Kwa jumla, kura za ‘ndiyo’ za Zanzibar zilikuwa ama 147 au 148 na ‘hapana’ ama saba au nane; wakati kwa matokeo ya Tanzania, wajumbe waliopiga kura walikuwa 335 na kura moja tu ndiyo ilikataa ibara zote na kura mbili zilichomoza kukataa baadhi ya ibara.
Matokeo hayo yalithibitishwa na mawakala Amina Makilagi na Waziri Rajabu Salum ambao walisimama na kueleza namna ambavyo kura hizo zilihesabiwa kwa uhuru mpana.
Kuserebuka bungeni
Baada ya matokeo hayo, Ukumbi wa Bunge ulihanikizwa kwa nyimbo za mipasho na mafumbo zikiambatana na kuwashwa vipaza sauti bila ya utaratibu na wajumbe kurukaruka na kukumbatiana kwa furaha.
Hali hiyo, iliwalazimu walinzi wa viongozi kuingia ndani ya ukumbi kwa kuweka hali ya amani kwani wajumbe walianza kuvamia viti vyao kwa nia ya kuwapongeza.
Hali ilipozidi, walinzi wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda walimwondoa haraka na kumweka katika chumba maalumu hadi hali ilipotulia huku idadi kubwa ya walinzi ikisogea kwa Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta.

Baada ya kuwatuliza, Sitta alisema walichokuwa wanafanya ni kuvunja kanuni, lakini kwa kuwa mwenyekiti naye alikuwa akicheza basi hakuna tatizo na amewasamehe.
Filikunjombe, Lugora wakwama
Wabunge wawili, Deo Filikunjombe (Ludewa- CCM) na Kangi Lugola (Mwibara-CCM) ambao hawakuwapo wakati wa mchakato, jana waliingia ukumbini lakini Sitta alitangaza kuwa haikuwapo tena nafasi ya kupiga kura.
“Nitangaze leo kuwa hakuna nafasi ya kupiga kura kwa wajumbe ambao hawakupata nafasi hiyo, nasema hivyo kwa kuwa matokeo yote tunayo hapa na hivyo hakuna sababu za kupiga kura tena,” alisema Sitta.
Wakati wa upigaji wa kura, majina ya wabunge hao yalipoitwa wajumbe waliitikia kwa sauti “ukawa haooo”.
Baada ya tangazo hilo, wabunge hao waliamua kuondoka ukumbini na kutokomea. Lugola hakupatikana kwa simu kuzungumzia hali hiyo lakini Filikunjombe alipokea simu na kusema alikuwa kwenye mkutano.
Ukawa: Harakati kuendelea
Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, Freeman Mbowe alisema harakati za kuipata Katiba bora yenye masilahi ya wananchi zitaendelea bila kusimama.
“Tumeona kichekesho na dhihaka iliyotokea Dodoma, kwa mustakabali wa Taifa hili. Ni vyema CCM wakawa makini kutotumia vibaya fursa hii ya kuiongoza nchi kwa kuzingatia hoja na matakwa ya kuipata Katiba, bila kutumia rushwa wala nguvu ya dola.
“Bado tunajadiliana ili tutoe tamko la pamoja. Rasimu iliyopitishwa ina maswali mengi kuliko majibu. Baada ya muda mfupi wa kujadiliana baina yetu tutasema msimamo wetu,” alisema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Issa Musoke alisema wananchi hawana sababu ya kuikubali rasimu iliyopitishwa kwa kuwa ni batili.
“Rasimu iliyopitishwa ni ya kamati ya uandishi na siyo ya Taifa hili kwa sababu imekiuka kanuni. Rais aliunda Tume ya kukusanya maoni ya wananchi ambayo yangejadiliwa katika Bunge Maalumu la Katiba, kama taratibu zilivyoainisha. Bunge hilo lilikuwa na jukumu moja la kutunga Katiba kutokana na maoni ya wananchi,” alisema na kuongeza:
“Watanzania tumekuwa waoga wa kupitiliza. Hatutaki kusema ukweli hata kama unahitajika. Kwa kilichofanyika ni kwamba wananchi hawakutendewa haki.”
Aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Humphrey Polepole alisema wajumbe wanafurahia kupitisha Katiba inayopendekezwa katika mazingira ya kushindwa.
“Wameshindwa kutupatia Katiba inayotokana na maoni ya Watanzania. Wametoa maoni ya wananchi na kuweka yao. Huwezi kupata Katiba nzuri kama hakuna maridhiano huku mijadala yote ikitawaliwa na itikadi za vyama vya siasa na mizengwe,” alisema.
Alisema kitendo cha Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Othman Masoud Othman kupiga kura ya ‘hapana’ kinaonyesha kuwa Zanzibar imegawanyika zaidi na hilo lilidhihirika baada ya mwanasheria huyo kutaka kupigwa na wajumbe wenzake kutoka huko.
Alisema wajumbe wa Tume hiyo wataendelea kuitetea Rasimu ya pili ya Katiba iliyotolewa na Tume hiyo kwa sababu ilitokana na maoni ya wananchi.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Masuala ya Ardhi (HakiArdhi), Yefred Myenzi alisema Katiba inayopendekezwa ni kichekesho kwa sababu licha ya kupingwa na wananchi wengi, imeongezwa sura mpya ya ardhi ambayo haijajibu mambo manne ya msingi kuhusu ardhi.
Alitaja mambo yaliyokosekana katika sura ya ardhi iliyoongezwa kuwa ni; kutoeleza ardhi inamilikiwa na nani, vyombo vya kusimamia ardhi, mfumo wa matumizi ya ardhi na uhusiano kati ya ardhi na rasilimali nyingine.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema, “Zoezi la upigaji kura lilikosewa na lilikosa uwazi, hasa kwa wajumbe waliopiga kura kwa njia ya faksi na baruapepe. Ilitakiwa tuelezwe idadi yao kamili pamoja na majina yao ili kujiridhisha kama kweli kura hizo siyo za maruhani.”
Aliongeza, “Kwa kutumia vyanzo vyangu nilifanikiwa kuona kura ya mmoja wa wajumbe waliopiga kwa njia ya mtandao. Kwa jinsi ilivyokuwa, ilikuwa rahisi kwa kura hizo kuchakachuliwa.”
Dk Slaa aliponda kitendo cha wajumbe wa Bunge hilo wakati wakipiga kura, kutamka kuwa wanapiga kura kwa niaba ya kundi fulani kwa sababu kitendo hicho ni kinyume na kanuni za uchaguzi ni sawa na kufanya kampeni.
“Wajumbe wa Bunge la Katiba pia walikosea sana kusema kuwa Katiba iliyopendekezwa imetambua haki za makundi yote bila kuwaeleza wananchi kuwa Ibara ya 20 ya Rasimu ya Katiba inakataza haki hizo kudaiwa mahakamani,” alisema.
Aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (Saut), Dk Charles Kitima alisema: “Katiba inayopendekezwa ina uhalali wa kisheria lakini inakosa uhalali wa wananchi.
“Haikuwa busara kupuuza maoni ya wananchi na Tume ya Katiba. Katiba hii imepitishwa kwa ubabe wa CCM na watu watambue kuwa siku wananchi wakipata fursa ya kujitawala kidemokrasia wataidai Katiba yao tu.”

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Ruaha, Profesa Gaudence Mpangala alisema: “Jambo la msingi si kupata theluthi mbili ya wajumbe kupitisha Katiba. Katiba lazima ipatikane kwa maridhiano na si kwa ubabe kama ilivyotokea Dodoma.
“Unaweza kutumia ubabe katika hatua ya kupiga kura kupitisha Katiba inayopendekezwa, lakini huwezi kutumia ubabe huo katika upigaji wa kura ya maoni. Tangu mwanzo nilipinga mchakato huu kwa sababu watu waligawanyika na ilitakiwa maridhiano yafanyike kwanza.”
Profesa wa Sheria UDSM, Chris Peter Maina alisema: “Utaratibu uliotumika utawagawa wananchi. Katiba haipatikani kwa namba, bali kwa maridhiano. Siombei mabaya lakini ukweli ndiyo huo, hii Katiba itatugawa na si jambo la kushangilia hata kidogo.”
Alisema Katiba inayopendekezwa ni dhaifu kwa sababu haina maoni ya msingi yaliyotolewa na wananchi ambayo yalikuwa katika rasimu iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo kwa miezi 20 ilifanya kazi ya kukusanya maoni ya wananchi.
Wakili Mwandamizi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Harold Sungusia alisema: “Nina uchungu sana kwa sababu kwa mara nyingine Tanganyika tumeizika. Hata hivyo, LHRC tunafanya tathmini ya mchakato mzima wa Katiba na tutatoa tamko rasmi.”

0 comments:

Post a Comment